top of page
Search
Leo Kilamile

Ndani ya Sekta ya Umma Tanzania - Dondoo kutoka Ripoti ya CAG ya mwaka 2022/23

Updated: 2 days ago

Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zilizochapishwa mwezi Aprili 2024 zilifichua maswala muhimu kuhusu hali ya kifedha ya Tanzania na utendaji wake wa sekta ya umma kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2023. Ripoti hizi ni muhimu katika kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali za umma.


Kifungu cha 56 cha Standadi ya Kuripoti Taarifa za Fedha ya Tanzania (TFRS 1) kinazitaka taasisi zote za umma na taasisi zenye maslahi ya Umma (PIEs) kuchapisha kwenye tovuti zao ripoti za waliokabidhiwa majukumu ya utawala wa taasisi pamoja na taarifa za fedha zilizokaguliwa si zaidi ya siku 30 baada ya kuidhinishwa kwa taarifa za fedha zilizokaguliwa.


Licha ya takwa hilo, mashirika kadhaa ya sekta ya umma bado hayajachapisha ripoti zao za 2022/23 kwenye tovuti zao. Sambamba na hilo, Wizara ya Fedha bado haijachapisha taarifa jumuishi ya fedha za 2022/23 kwenye tovuti.

Kanuni ya Uwazi wa Fedha ya IMF inasema, pamoja na mambo mengine, 'Ripoti za Fedha [Taarifa za fedha za mwaka zilizokaguliwa] zinapaswa kuchapishwa mara kwa mara, na kwa wakati'. Kuchapisha taarifa za fedha ndani ya muda husaidia kuzifanya ziwe na umuhimu kwa watumiaji.

Yawezekana wakati umewadia kwa serikali kuanza utaratibu wa uchapishaji wa taarifa za fedha jumuishi kwa wakati pamoja na taarifa za fedha za mashirika mengine ya umma ili kuboresha umuhimu wa taarifa, kuzingatia kanuni za uwazi, na zaidi sana, kutii matakwa ya standadi yetu wenyewe (TFRS 1).


Andiko hili litaangazia maswala ya sekta ya umma yatokanayo na ripoti za CAG. Maboresho zaidi yanaweza kufanywa baada kuchapishwa kwa taarifa zaidi za kifedha.

 

PERUZI KWA HARAKA (Bonyeza ">" kuona zaidi)

 

SEHEMU YA 1: Hali ya Ukusanyaji wa Mapato


Kiasi gani kilikusanywa?


Moja ya mambo muhimu yaliyoangaziwa katika taarifa za fedha ni utendaji wa jumla wa ukusanyaji wa mapato. Tanzania ilirekodi ongezeko la ukusanyaji wa mapato, kwa kukua kwa 9%  ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliotangulia (2021/22).


Kwa mwaka 2022/23, Serikali ilikusanya TZS 41.88 trilioni, sawa na 100.96% ya makadirio yaliyopangwa ya TZS 41.48 trilioni. Kwa hiyo, kulikuwa na makusanyo ya kupita makadirio ya TZS 400 bilioni, ikiwa ni takriban 0.96% ya makadirio ya makusanyo.


Makusanyo ya Serikali kwa mwaka 2022/23 (Viwango kwa TZS trilioni)

Aina ya Mapato

Halisi 2022/23

Bajeti 2022/23

Asilimia kulinganisha na Bajeti

Makusanyo Mwaka Uliopita

Mabadiliko kwa Mwaka %

Kodi

22.583

23.652

95.48%

20.945

7.82%

Makusanyo yasio kodi

2.7095

3.352

80.83%

2.709

0.02%

Mapato ya Serikali za Mitaa

1.222

1.012

120.75%

0.892

37.00%

Mikopo ya Ndani

6.124

5.780

105.95%

6.489

-5.62%

Misaada

0.759

1.101

68.94%

1.305

-41.84%

Mikopo ya Nje ya Masharti nafuu

5.523

3.547

155.71%

4.149

33.12%

Mikopo ya Nje ya Masharti ya kawaida

2.959

3.034

97.53%

1.809

63.57%

JUMLA

41.88

41.48


38.298


Mapato yaliyokusanywa juu ya makadirio yalichangiwa zaidi na makusanyo ya ziada ya takribani TZS 2 trilioni kutoka kwenye Mikopo ya Nje ya masharti nafuu.


1.1         Mgawanyo wa vyanzo vya mapato yaliyokusanywa (TZS 41.88 trilioni)

Chanzo kikuu cha makusanyo ya mapato kilikuwa ni kodi (54%), ikifuatiwa na mikopo ya ndani (15%) na mikopo ya masharti nafuu kutoka nje (13%).


Tazama chati hapa chini:

Tanzania Sources of Revenue
Vyanzo vya Mapato - Tanzania 2022/23

1.2         Mapato kwenda Mfuko Mkuu wa Fedha wa Hazina

Ibara ya 135 ya Katiba ya Tanzania inataka mapato yote ya Serikali yawekwe kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina.


Kati ya TZS 41.88 trilioni zilizokusanywa, TZS 38.447 trilioni ziliwekwa katika Mfuko Mkuu wa Hazina. TZS 3.433 trilioni (sawa na 8.2% ya makusanyohazikuwekwa. CAG anafafanua zaidi kuwa pamoja na fedha hizo kutowekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, zilikaguliwa na kuripotiwa kupitia ripoti za miradi husika.


1.3         Maswala Mengine kuhusu Utendaji wa Ukusanyaji wa Mapato

a)    Katika miaka mitano (5) ya hivi karibuni, uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa kwa Tanzania umesalia chini kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki (Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi). Hiyo ina maana, ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki, sehemu ndogo ya jumla ya pato la taifa inakusanywa kama kodi. Uwiano wa Kodi kwa Pato la Taifa kwa Tanzania umekuwa kati ya 11.70% hadi 12.80%; huku Kenya (13.7% - 15.5%), Uganda (12.1% - 15.1%), Rwanda (15% - 16.3%), na Burundi (15.2% - 18%).


b)    Mapato ya ushuru kiasi cha TZS 10.489 Trilioni yapo kwenye kesi zinazosubiri maamuzi kwenye mahakama za kodi kutokana na sababu kadhaa zinazoathiri mifumo ya rufani. Hata hivyo, haikuelezwa kama Mamlaka ya Mapato (TRA) ilifanya tathmini ya maamuzi ya mahakama ili kujua uwezekano na asilimia ya Serikali ya Tanzania kushinda.


c)    49% ya walipa kodi waliosajiliwa na VAT katika mikoa tisa (9) ya kodi hawakuwasilisha ritani za VAT.


d)    Mapungufu katika usimamizi wa mapato yasiyo ya kodi ikijumuisha, utendakazi duni wa kutoa huduma, kodi za nyumba kutoka kwa taasisi za serikali na watumishi wa umma ambazo hazijakusanywa (4.8B), mapato ambayo hayakutozwa (768M), mapato yasiyokusanywa (61B), pesa iliyokaa bila kazi (4B), n.k.


1.4         Usimamizi wa Mapato na Mashirika ya Umma


Katika mwaka 2022/23, CAG pia alifanya kaguzi kwa mashirika ya sekta ya umma (PSEs) 215. Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu yaliyobainishwa kuhusu usimamizi wa mapato wa baadhi ya PSEs:


i. Mashirika 66 ya sekta ya umma kati ya mashirika 215 yaliyotengewa bajeti ya kukusanya mapato ya TZS 799.09 bilioni yalikusanya TZS 514.39 bilioni (64%) na kusababisha upungufu wa TZS 284.71 bilioni (36%).


ii. Mashirika 66 ya umma yalikuwa na madeni makubwa ambayo hayajalipwa ya jumla ya TZS 2.92 trilioni, yanayohusiana na huduma zinazotolewa kwa wateja na hayakulipwa kwa muda wa zaidi ya miezi 12. Taasisi kumi (10) zilizoongoza kwa kiasi kikubwa cha fedha ambazo hazijalipwa ni HESLB (808B), TPDC (475B), TANESCO (435B), MSD (366B), NHIF (208B), TTCL (107B), TPA (93B), TCRA. (57B), TMDA (35B), na CDTF (34B).


iii. Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira zilipoteza maji yenye mapato yenye thamani ya TZS 162.25 bilioni kabla ya kuwafikia wateja. TZS 162.14 bilioni zilipotea katika mwaka uliotangulia (2021/22).


Kwa mujibu wa EWURA, upotevu wa maji unaovumilika (maji yasiyo ya mapato) haupaswi kuzidi 20%; lakini, mamlaka 30 za maji zilikuwa na maji yasiyo ya mapato zaidi ya 20%. Miongoni mwao, mamlaka nane (8) za maji zilipata upotevu wa maji zaidi ya 40%; ambazo ni Kyela-Kasumulu (41%), Dar-es-salaam (42%), Karatu (45%), Korogwe (45%), Arusha (46%), Mtwara (48%), Ngara (48%), na Kigoma (65%).


iv. Kulikuwa na mapungufu katika urejeshaji wa madeni kwa Mamlaka za Maji. Kwa mfano, mamlaka za maji za DAWASA, Arusha, na Mtwara zilikuwa na wateja wenye bili ambazo hazijalipwa za TZS 10.87 bilioni, TZS 809.2 milioni na TZS 1 bilioni mtawalia. Wateja hao hawakukatiwa huduma.


 

SEHEMU YA 2: Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma


Kiasi gani kilitumika?


TZS 39.523 trilioni zilitolewa kwa ajili ya matumizi kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina. Matumizi hayo yalizidi Mapato yaliyowekwa kwa TZS 1.742 trilioni (sawa na asilimia 4.5), na hivyo kusababisha malipo ya ziada hadi tarehe 30 Juni 2023.


2.1       Mgawanyo wa Fedha Kutoka Hazina

Kati ya TZS 39.523 trilioni zilizotolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali, TZS 31.917 trilioni (80.8%) zilitolewa kwa Taasisi za Serikali Kuu, na TZS trilioni 7.606 (19.2%) zilitolewa kwa Serikali ya Mitaa (OR-TAMISEMI).


Tunaweza elewa kwamba fedha zilizotolewa kwa Mashirika ya Serikali Kuu zilijumuisha fedha zilizotumika kulipa Deni la Umma. Kiasi halisi hakikutajwa kwenye ripoti ya jumla ya CAG. Kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni 2022, fedha zilizotumika kwa deni la umma zilikuwa TZS 10.4 trilioni. Jedwali hapa chini linaonyesha mgawanyo wa fedha zilizotolewa kwa ajili ya matumizi.


Mgawanyo wa Fedha zilizotolewa (viwango kwa TZS trilioni)

Fedha Kwenda kwa:

MATUMIZI YA KAWAIDA

MATUMIZI YA MAENDELEO

JUMLA

Serikali Kuu na Taasisi

20.99*

10.927

31.917

Serikali za Mitaa

5.206

2.4

7.606

JUMLA

26.196

13.327

39.523

*Matumizi ya kawaida ya Serikali Kuu yaweza kuwa yamejumuisha fedha zilizotolewa kwa ajili ya Kuhudumia deni la umma.


Je, fedha hizo zilitumikaje?


2.2         Matumizi ya Serikali Kuu na Taasisi zake

Kama ilivyoelezwa hapo awali, Serikali Kuu na Taasisi zake [i.e. Wizara, Wakala, Taasisi na Idara, ikijumuisha Fungu la Deni la Umma] zilipokea TZS 31.917 trilioni, 80.8% ya fedha zote zilizotolewa kutoka kwa Mfuko Mkuu wa Serikali.


Kati ya fedha zilizopokelewa, taasisi za serikali kuu zilitumia TZS 31.823 trilioni, ambayo ilikuwa 99.7% ya fedha iliyotolewa; hivyo, TZS 94 bilioni hazikutumika na zilirudishwa kwa mlipaji mkuu wa Serikali (PMG).


Yafuatayo ni baadhi ya maswala yaliyoibuliwa na ukaguzi wa CAG kwa Serikali Kuu:


a)    Taasisi nne (4) za serikali zilitumia TZS 10.20 bilioni kwa matumizi ya kawaida na ya maendeleo nje ya bajeti zao zilizoidhinishwa.


b)    Taasisi 13 za Serikali zilifanya Malipo ya jumla ya TZS 2.87 bilioni bila kudai risiti za EFD.


c)    TZS 1.78 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa Kamisheni ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda zilibaki bila kutumika kwa miaka mitano kuanzia tarehe 4 Julai 2018 hadi 30 Juni 2023. Kwa upande mwingine, Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa mjini New York ulitumia fedha za amana kiasi cha TZS 675 milioni bila kibali kwa sababu ya wizara haikutoa fedha.


d)    Gharama kubwa za kupangisha zinazolipwa na balozi za Tanzania Nje ya Nchi - Kodi kwa mwaka za TZS 1.58 bilioni, TZS 1.42 bilioni, na TZS 1.19 bilioni zililipwa na Balozi za Tanzania huko Moscow, Abu Dhabi na Vienna, mtawalia. Balozi zinaonekana kutokuwa na mpango wa kupunguza gharama.


e)    Jumla ya gharama ya kandarasi ya kukarabati jengo kuu la zamani huko Washington DC, Marekani ilikuwa mara mbili ya makadirio ya Mhandisi. Mhandisi alikadiria TZS 5.98 bilioni, wakati jumla ya kandarasi ilikuwa TZS 11.57 bilioni.


Katika mradi huo, CAG aliona yafuatayo:

  • Kiasi cha Mkataba kilijumuisha Dola 357,428.58 kwa huduma ambazo tayari zimetolewa na Wizara katika mkataba na mshauri mwingine.

  • Kulikuwa na utozaji mara mbili wa Tozo za Mamlaka za Mitaa za Dola 170,204.07.

  • Kiwango cha VAT huko Washington ni 6%, lakini kiwango kilichotozwa katika mkataba kilikuwa 20%. TZS 153.99 milioni tayari zililipwa kama VAT kulingana na kiwango cha 20%.

  • Kulikuwa na Gharama za Ziada ambazo hazijaidhinishwa za Dola 418,790.

  • Makampuni yaliyoorodheshwa kwa zabuni hayakufanyiwa tathmini ya uwezo wao.

  • Mradi haukuwepo katika Mpango wa Manunuzi wa Mwaka ulioidhinishwa.


f)     TANROADS ilitozwa riba ya TZS 34.82 bilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 kutokana na kuchelewa kuwalipa makandarasi na washauri wa miradi ya ujenzi wa barabara.


g)    Pesa baada ya Usuluhishi yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 12 haijalipwa tangu 2014, na kulimbikiza tozo za riba za TZS 17.48 bilioni hadi tarehe 30 Juni 2023.


h)    RUWASA ilitoa Zabuni kwa bei iliyokuwa mara saba (7) zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa. Bajeti iliyoidhinishwa ilikuwa TZS 45.3 bilioni na zabuni zilitolewa kwa TZS 317.75 bilioni.


i)      Mfuko wa Dhamana wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) ulitarajia hasara katika mikopo iliyotolewa ya TZS 20.43 bilioni, ambayo ni asilimia 80 ya mikopo ambayo haijalipwa (25.42B) kufikia tarehe 30 Juni 2023.


j)     Serikali haijairejesha NSSF TZS 215 bilioni kwa ajili ya Ujenzi wa Daraja la Nyerere (Kigamboni) kama sehemu ya mchango wao. Riba ya ziada ya TZS 26.88 bilioni ilitozwa hadi tarehe 30 Juni 2023.


k)    Jeshi la Polisi la Tanzania limekuwa na Madeni ya Muda Mrefu ya Dola za Kimarekani tangu mwaka 2015. Kwa sababu ya mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha, thamani ya deni katika TZS sasa imeongezeka kwa TZS 24.10 bilioni, ikiwa ni nyongeza ya 10% ya deni la awali la TZS.


l)      Dawa katika hospitali 10, zenye thamani ya TZS 1.99 bilioni, zilipatikana kuwa zimeisha muda wa matumizi hadi miaka 18 lakini hazikutupwa na hospitali husika.


m)  Makampuni ya uuzaji wa Mafuta yalinufaika na TZS 18.94 bilioni zilizokusanywa kutoka kwa umma ambazo zilipaswa kulipwa kwa wasambazaji wa Mafuta kama ada ya ucheleweshaji.



2.3         Matumizi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa

Kama ilivyoelezwa hapo awali, Mamlaka za Mitaa [i.e. OR-TAMISEMI, RAS, na LGA] zilipokea TZS 7.606 trilioni, 19.2% ya fedha zote zilizotolewa kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.


Pesa zilizopokelewa na Serikali za Mitaa ni 86% ya matarajio (8.82T). Upungufu huo ulijitokeza zaidi katika Bajeti ya Maendeleo kuliko Bajeti ya Matumizi ya Kawaida. Fedha za matumizi ya kawaida zilizopokelewa ni 94% ya bajeti, huku fedha za maendeleo zilizopokelewa zikiwa 73% ya bajeti.


Upungufu katika bajeti ya maendeleo ulionekana zaidi katika bajeti mahususi za mikoa. Kwa upande wa Wizara (OR-TAMISEMI) ilipokea 99% ya bajeti yake ya maendeleo.


Mikoa iliyopata zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya maendeleo ni Songwe (75%), Mwanza (75%), Pwani (78%), DSM (79%) na Geita (80%).


Mikoa iliyopata chini ya asilimia 55 ya bajeti ya maendeleo ni Lindi (55%), Singida (54%) na Dodoma (51%).


2.3.1   Mgao wa Fedha kwa Mikoa

Asilimia 89 ya fedha yote iliyotengwa kwa Serikali za Mitaa ilisambazwa kwa mikoa 26 ya Tanzania Bara. Asilimia 11 iliyobaki ilitolewa moja kwa moja kwa Wizara ya Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya kufadhili Miradi ya Maendeleo.


Asilimia 53 ya fedha za mikoa zilipelekwa kwa mikoa 10: Dar-es-salaam (576B), Mwanza (444B), Morogoro (366B), Tanga (337B), Arusha (330B), Mbeya (326B), Kagera (308B), Pwani (308B), Kilimanjaro (293B), na Dodoma (290B).


Mikoa 10 iliyopata mgawo mdogo (25% ya fedha zilizotolewa) ni Mtwara (206B), Iringa (205B), Shinyanga (199B), Singida (189B), Simiyu (186B), Njombe (175B), Songwe (165B), Lindi (148B), Rukwa (131B), na Katavi (105B).


2.3.2   Ulinganisho wa uwezo wa Ukusanyaji wa Mikoa na Mgao wa Fedha toka Hazina

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Makusanyo ya Mapato ya Ndani kutoka Mikoa kwa mwaka 2022/23 yalikuwa TZS 5.3 trilioni. Vilevile, kwa mwaka 2022/23 Halmashauri ziliripoti makusanyo ya vyanzo vyake ya TZS 1.2 trilioni, na kufanya jumla ya makusanyo ya ndani kutoka kwa mikoa kuwa TZS 6.5 trilioni.


Mbali na makusanyo ya ndani, TRA pia iliripoti mapato zaidi ya TZS 18.4 trilioni (yaani TZS 9.35 trilioni kutokana na ushuru wa forodha na TZS 9.05 trilioni kutoka kwa Walipakodi Wakubwa). N.B: Kwa sababu za kiutawala kwenye usimamizi wa kodi, kodi kutoka kwa Walipakodi Wakubwa huwa hairipotiwi kama sehemu ya makusanyo ya kodi kutoa mikoa husika walipo walipakodi.


Kwa kuwa jumla ya mgao wa fedha kwenda kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ulikuwa TZS 7.606 trilioni, inamaanisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizidishiwa TZS 1.106 trilioni zaidi ya jumla ya makusanyo yao ya ndani. Kiasi cha ziada ni sawa na 6% ya jumla ya makusanyo mengine ya TRA kutoka kwa ushuru wa Forodha na walipakodi Wakubwa.


Hii inaweza kuwa inamaanisha nini?
Kodi za ndani zilizokusanywa kutoka kwa walipakodi wakubwa (ambao pia wamo ndani ya mamlaka za mikoa mbalimbali) hazikurejeshwa moja kwa moja kwa mikoa husika, bali zilitumika zaidi kugharamia bajeti ya Serikali Kuu. Pia inamaanisha, kuna mchango mdogo sana wa makusanyo ya kodi ya forodha kwa bajeti za mikoa.

2.3.3   Maswala mengine kuhusu Matumizi ya Serikali za Mitaa

Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu kutoka ripoti ya ukaguzi wa CAG kwa Mamlaka za Mitaa:


a)    Fedha za miradi zenye jumla ya TZS 7.73 bilioni katika Halmashauri 25 zilichepushwa kufadhili miradi mingine na matumizi ya kawaida.


b)    Kughushi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe kwa kuwasilisha kumbukumbu za kughushi za kikao cha kamati ya fedha, utawala na mipango. Hati ya kughushi ilitumika kubadili bajeti ya mishahara ya watu kwa kuongeza TZS 2 bilioni.


Pia, katika wilaya hiyo hiyo malipo ya jumla ya TZS 1.23 bilioni yalifanywa kwa shughuli mbalimbali ambazo hazikufanyika na hayakugundulika na mifumo ya ndani ya udhibiti na uhasibu.


c)    Madai ya riba yaliyolimbikizwa ya TZS 2.23 bilioni kwa kuchelewesha malipo ya Wakandarasi. Ucheleweshaji wa malipo ulisababishwa na kucheleweshwa kwa utoaji wa fedha za mradi kulikosababishwa na Wizara ya Fedha.


d)    Halmashauri tisa (9) zilinunua vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya TZS 868.43 milioni  zaidi ya kiasi kinachohitajika kwa ajili ya miradi husika, na hivyo kupelekea vifaa hivyo kubaki bila kutumika.


e)    TZS 7.42 bilioni zililipwa na Halmashauri 65 kwa wazabuni, wakandarasi na watoa huduma wengine bila kudai risiti za EFD.


f)     Halmashauri 23 zililipa jumla ya kiasi cha TZS 787.49 milioni kwa matumizi ambayo hayakuwa na maana.


g)    Mamlaka za Serikali za Mitaa zilifanya malipo kwa fedha taslimu  kiasi cha TZS 1.44 bilioni. Hiyo ni kinyume na Aya ya 6.7.3 ya Mwongozo wa Uhasibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, 2019 unaozitaka halmashauri kufanya malipo yote kwa njia ya kielektroniki na kuelekeza kwenye akaunti za benki za mlipwaji, na, kwa hali yoyote halmashauri haipaswi kulipa kwa hundi au fedha taslimu.


h)   Halmashauri 43 zilikata kodi ya zuio kutoka kwa wazabuni ya TZS 1.74 bilioni, lakini hazikuwasilishwa TRA.                             


i)      Wanufaika wa mikopo katika Halmashauri 151 walishindwa kulipa jumla ya TZS 79.76 bilioni. Pia, Halmashauri 46 zilikuwa na mikopo ambayo haijalipwa ya jumla ya TZS 5.70 bilioni kutoka kwa vikundi 1,334 ambavyo tayari vilikuwa vimeacha kufanya biashara. Zaidi ya hayo, CAG hakuweza kuthibitisha kuwepo kwa vikundi 850 katika Halmashauri 18 zilizoripoti kutoa mikopo ya jumla ya TZS 2.6 bilioni.


2.4         Matumizi ya Mashirika ya Umma


Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu kutoka ripoti ya CAG katika Mashirika ya Umma:


a)    Kwa upande wa TPA, gharama za ziada za TZS 808.85 milioni na Euro 4.84 milioni zilisababishwa na ucheleweshaji wa kukamilisha mikataba. TPA haikuweza kufanya malipo ya awali kwa wakati na kutoa barua ya udhamini hivyo kuchelewesha kuanza kwa mkataba na kusababisha ongezeko la gharama za mkataba.


b)    MSD ilipata hasara ya TZS 1.99 bilioni katika ununuzi wa vitendanishi ambavyo havikidhi masharti ya kiufundi.


c)    Kuingiliwa kwa mchakato wa ununuzi na Wizara ya Maliasili na Utalii kulisababisha gharama ya ziada ya TZS 702.68 milioni katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA)


d)    Matumizi yasiyo na tija na ya hovyo ya TZS 72.36 bilioni ambapo mashirika 17 hayakupata thamani ya fedha.


e)    Taasisi 11 zilifanya matumizi yasiyostahiki ya jumla ya TZS 4.64 bilioni.


f)     Malipo ya udanganyifu ya TZS 58.94 milioni yaliyofanywa kupitia MUSE katika Taasisi ya Maendeleo na Mipango Vijijini (IRDP).


g)    Mashirika 16 kati ya 215 yaliyokaguliwa hayakuwasilisha kodi mbalimbali za TZS 33.45 bilioni kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kinyume na sheria za kodi.


h)    Mashirika tisa (9) ya sekta ya umma yalifanya malipo ya bidhaa na huduma ya jumla ya TZS 2.17 bilioni ambayo hayakuambatanisha na risiti za EFD.


 

SEHEMU YA 3: Utendaji na Utoaji Huduma wa Mashirika ya Umma


3.1         BENKI

CAG alipitia benki tatu (3) za biashara za serikali (TIB Development Bank, Azania Bank na Tanzania Commercial Bank (TCB)).


a)    Benki mbili (TIB Development Bank na Azania Bank) zilivuka kiwango kinachokubalika cha Mikopo iliyochacha (NPL) cha asilimia 5 iliyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania. Uwiano wa NPL katika Benki ya Maendeleo ya TIB ulikuwa 21.50% (2022: 20.28%) wakati katika Benki ya Azania ilikuwa 7.44% (2022: 18.25%).


b)    TCB ilitoa mikopo iliyozidi kiwango cha TZS 734.28 bilioni bila idhini ya bodi.



3.2         MIFUKO YA PENSHENI

a) Kiwango cha ukwasi cha PSSSF kiko chini ya kiwango kilichopendekezwa. Hayo ni kwa mujibu wa Tathmini ya Kitaalamu ya Mfuko iliyofanyika. Kiwango cha sasa ni 22.30% ambacho kiko chini ya kiwango kilichopendekezwa cha 40%.


CAG pia aliripoti usimamizi duni wa Uwekezaji wa mifuko ya pensheni, kama vile:


b)    Ukusanyaji usioridhisha wa kodi za pango kwa mali za uwekezaji za NSSF, PSSSF, na NIC TZS 47.10 bilioni


c)    Utendaji usioridhisha wa Kilimanjaro Leather Industry Company Limited (KLICL)


d)    Mapungufu katika kusimamia Mkulazi Holding Company Limited yenye mtaji uliowekezwa TZS 312.98 bilioni.


e)    Kutokuwa na uhakika juu ya urejeshwaji wa kodi inayodaiwa na Ubungo Plaza Limited TZS 10.98 bilioni



3.3         ELIMU

a) Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kina upungufu mkubwa wa maji wa lita milioni 1.1 kwa siku, sawa na 49% ya makadirio ya mahitaji. UDOM ina wastani wa watu 38,203 wanaojumuisha wafanyakazi na wanafunzi.


b)    Upungufu wa vifaa vya maktaba katika vyuo vikuu na taasisi nyinginezo za kitaaluma


c)    Bodi ya Mikopo (HESLB) ilikuwa na mikopo iliyoiva ya TZS 2.10 trilioni na iliweza kukusanya TZS 1.29 trilioni (62% ya mikopo yote iliyoiva) kuanzia 2006/07 hadi 2022/23. Hii ina maana kwamba TZS 0.81 trilioni, 38% ya mikopo iliyoiva haikukusanywa kufikia tarehe 30 Juni 2023.



3.4         AFYA

a)    NHIF ilikataa bili za hospitali zenye thamani ya TZS 20.77 bilioni.


NHIF ilikataa jumla ya TZS 11.83 bilioni sawa na 15% ya jumla ya madai ya TZS 76.89 bilioni kutoka Taasisi nne (4) za Muhimbili (MNH-Mloganzila, MNH, MOI, na MUHAS). Sababu kuu za kukataliwa ni madai ya uwongo na kutokuwepo kwa misingi ya uhalali kwa kutofuata sheria au kanuni zinazohusiana na malipo ya madai, madai mara mbili, matumizi makubwa ya huduma, kutozingatiwa kwa bei ya NHIF, huduma ambazo hazijaonyeshwa katika uchunguzi, ukosefu wa huduma. au ubatili wa nambari za uidhinishaji, kukosa maelezo ya huduma zinazodaiwa baada ya kuthibitishwa, kutokuwepo au kutokuwa sahihi kwa saini za mgonjwa, huduma zisizo ndani ya kifurushi cha manufaa cha NHIF, makosa ya hesabu, kuagiza kupita kiasi, na kutofuata miongozo ya kawaida ya matibabu.


NHIF pia ilikataa madai ya TZS 8.94 bilioni kutoka Hospitali nyingine 24 za Rufaa za Mikoa (RRH) kutokana na makosa mbalimbali, kama vile idhini batili, kanuni za magonjwa zisizofaa, na kutofuata miongozo ya kawaida ya matibabu. Madai yaliyokataliwa yalikuwa 13% ya madai yote yaliyowasilishwa na Hospitali za Rufaa za Mikoa.


b)    CAG alitaja mambo manne (4) yanayotishia uhai wa NHIF, ambayo ni:


  1. Madeni ya Serikali yasiyolipwa ya TZS 208 bilioni

  2. Mafao ya Wastaafu ambayo hayakulipiwa ambayo wastani wa matumizi ya kila mwaka ni TZS 84.70 bilioni

  3. Kupanda kwa gharama zinazohusiana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCD). Wastani wa matumizi ya mwaka kwa NCD ni TZS 137.80 bilioni

  4. Hali ya uhiari ya uanachama, ambapo watu hujiunga tu wakati wanahitaji huduma ya matibabu ya gharama kubwa.


3.5         MAENEO MENGINE

CAG aliona hatari ya kufeli kwa mradi wa makazi mapya ya jamii ya wazawa katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Hatari hiyo ilisababishwa na bajeti ya uhamisho (TZS 287 bilioni) ambayo haitokani na makadirio ya mtaalamu.


Mfano mmoja uliotajwa:- makadirio ya bajeti ya uhamisho yaligharimu TZS 9.97 milioni kwa kila nyumba, lakini mkataba halisi na mkandarasi (SUMA JKT) yalikuwa TZS 19.48 milioni kwa nyumba (zaidi ya mara mbili ya gharama iliyokadiriwa).


CAG aliishauri serikali kuandaa na kutekeleza mpango wa kina wa utekelezaji wa mradi na mkakati ili kuhakikisha mradi wa makazi mapya unakamilika kwa mafanikio.


3.6         MUHTASARI WA JUMLA WA UTENDAJI WA FEDHA wa MASHIRIKA YA UMMA (PSEs)


3.6.1   Mashirika ya Umma yenye Mtaji Hasi

Kati ya Mashirika 215 ya Umma, 11 (5%) yalikuwa na mtajji hasi (yaani, Madeni Zaidi kuliko Mali).


Jumla ya mtaji hasi kwa mashirika yote 11 ilikuwa TZS 503 bilioni, kati ya hizo 98.86% (TZS 497.2 bilioni) ilichangiwa na taasisi nne (4)  kama inavyoonyeshwa kwenye jedwali hapa chini (kiasi chote ni TZS bilioni):

SN

Taasisi

Aina

Mali

Madeni

Mtaji

1

Tanzania Fertilizer Regulatory

Authority

Sio Biashara

6.5

262.5

-256

2

Air Tanzania Company Limited

Biashara

339.4

553.7

-214.4

3

Cotton Development Trust Fund

Sio Biashara

148.4

168.3

-19.9

4

STAMIGOLD Company

Biashara

68

74.9

-6.9

 

 

 

562.3

1059.4

-497.2

3.6.2   Mashirika ya Kibiashara ya Umma (CPSEs) yenye Hasara Mfululizo

Mashirika 11 yaliripoti hasara katika miaka mfululizo. Mashirika matano ya juu yalichangia 97% ya jumla ya hasara ya mashirika yote yaliyopata hasara. Orodha ya taasisi imetolewa hapa chini (kiasi chote ni TZS bilioni):

SN

Taasisi

Hasara ya 2021/22

Hasara ya 2022/23

1

Tanzania Railway Corporation

190

100.7

2

TANOIL Investment Limited

7.8

76.6

3

Air Tanzania Company Limited

35.2

56.6

4

Kariakoo Market Corporation

0.5

41.6

5

Tanzania Biotech Products Limited

3.9

6.1

 

 

 

281.6

3.6.3   Mashirika Yasiyo ya Kibiashara ya Umma (NCPSEs) yenye Nakisi Mfululizo

Mashirika 23 yaliripoti nakisi katika miaka mfululizo. Mashirika matano 5 yenye nakisi kubwa zaidi yalichangia 95.9% ya jumla ya nakisi za mashirika yote. Orodha ya taasisi imetolewa hapa chini (kiasi chote ni TZS bilioni):

SN

Taasisi

Nakisi 2021/22

Nakisi 2022/23

1

National Health Insurance Fund

206

156.8

2

University of Dar es salaam

15.3

12.6

3

Mbeya Water Supply and Sanitation Authority

0.06

3.2

4

Petroleum Upstream Regulatory Authority

0.4

2.2

5

Tanzania Education Authority

5.5

1.7

 

 

 

176.5

3.6.4   Mashirika ya Umma yanayofadhiliwa na Madeni Makubwa


Kati ya Mashirika 215 ya Sekta ya Umma, 28 (13%) yalifadhiliwa na deni zaidi kuliko mtaji. Kati ya mashirika 28, 10 yalifadhiliwa na deni kwa zaidi ya mara tatu (3X) ya mtaji wao.


Mashirika yenye uwiano mkubwa wa madeni zaidi ya mtaji ni Shirika la Reli Tanzania (82X), RU Built Environment Consulting Company Ltd (14X), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (14X), Arusha Water Supply and Sanitation (4X), MCB Company Limited (4X), Bodi ya Rufaa ya Mapato Tanzania (4X), Watumishi Housing Investments (4X), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (4X), Mamlaka ya Rufaa ya Ununuzi wa Umma (3X), na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (3X).


Kwa kulinganisha kwa kiasi cha fedha, mashirika manne (4) yafuatayo yalikuwa na madeni makubwa zaidi ya mitaji yao: Shirika la Reli Tanzania (TZS 11.4 trilioni), TANESCO (TZS trilioni 9.6), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TZS 0.82 trilioni), na Mamlaka ya Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Arusha (TZS 0.37 trilioni).


CAG alifafanua kuwa; mashirika yenye madeni makubwa zaidi ya mitaji kwenye kufadhili mali zao yanakuwa wenye viashiria vya hatari ya kifedha inayotokana na gharama kubwa ya madeni.


 

SEHEMU YA 4: Je, Ripoti ya CAG ina Umuhimu na inaleta Manufaa?


Standadi ya Kimataifa - ISSAI 12, "Thamani na Manufaa ya Taasisi Kuu za Ukaguzi - kuleta utofauti kwa Maisha ya Raia," inasisitiza kwamba ripoti za ukaguzi zinapaswa kutolewa kwa wakati ili kuhakikisha umuhimu na manufaa. Inasisitiza kwamba mawasiliano kwa wakati ya matokeo ya ukaguzi huwezesha taasisi zilizokaguliwa na washikadau wengine kuchukua hatua za haraka za kufanya marekebisho, na hivyo kuimarisha uwajibikaji na uwazi. Vilevile, ISSAI 3000 na ISSAI 3100 (Standadi za Ukaguzi wa Ufanisi), zote zinasisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa wakati ili kuhakikisha kuwa matokeo ya ukaguzi yanaleta manufaa na yanapelekea kuboresha ufanyaji wa maamuzi na maboresho. Utoaji wa ripoti kwa wakati ni muhimu kwa kufanya maamuzi sahihi na kudumisha imani ya umma.


Hali ilivyo sasa

Nchini Tanzania, mwaka wa fedha unaisha tarehe 30 Juni. Taasisi za umma zina miezi mitatu, hadi tarehe 30 Septemba ili kuandaa na kuwasilisha taarifa zao za fedha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ukaguzi. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anapewa muda wa miezi sita hadi Machi 31, mwaka unaofuata, kuwasilisha ripoti za ukaguzi kwa rais. Ndani ya wiki moja hadi mbili, rais/serikali inatakiwa kuwasilisha taarifa hizi Bungeni, na kuzifanya kuwa nyaraka za wazi kwa umma.


Kufuatia hayo, Bunge linaiagiza serikali kuandaa majibu, mchakato unaochukua takribani miezi saba (Aprili hadi Oktoba). Katika kikao cha Bunge cha mwezi Novemba, ripoti za CAG hujadiliwa na bunge linaweza kutoa maazimio. Mchakato huu unamaanisha kuwa inachukua takriban miezi 17 kutoka mwisho wa mwaka wa fedha kwa matokeo ya ukaguzi kujadiliwa Bungeni. Pia ina maana kwamba hadi wakati mapendekezo ya CAG yanajadiliwa, serikali inaweza kuwa tayari imerudia makosa yale yale kwa mwaka mwingine ulioisha, hivyo kupunguza ufanisi wa ripoti hiyo katika kuboresha utendaji kazi wa serikali.


Muda mrefu kama huo unaweza kupunguza umuhimu na nguvu ya ripoti za CAG, kwani masuala yaliyoainishwa yanaweza kuwa yamepitwa na muda au yamezidi kuwa mabaya zaidi bila kushughulikiwa kwa wakati. Inatatiza uwezo wa Bunge kuwajibisha taasisi za umma na inaweza kupunguza ubora wa hatua za marekebisho. Muda wa kujadili matokeo ya ukaguzi ni muhimu ili kuhakikisha kwamba mapendekezo yanatekelezwa kwa haraka, kudumisha imani ya umma, na kuongeza uwazi na uwajibikaji wa usimamizi wa fedha za umma.

Tanzania's Financial Reporting Timeline
Nini kifanyike?

Ili kuboresha muda na ufanisi wa ripoti za ukaguzi nchini Tanzania, ni muhimu kupitia upya mchakato wa sasa wa kuripoti. Kwanza, muda wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukamilisha ukaguzi unaweza kufupishwa kwa kuboresha ugawaji wa rasilimali, kuhusisha makampuni binafsi ya ukaguzi, na kutumia teknolojia ili kuharakisha michakato ya ukaguzi.


Zaidi ya hayo, muda wa serikali kuandaa majibu unaweza kufupishwa zaidi ili kuwezesha majadiliano ya awali ya bunge. Hili linawezekana kwa sababu, wakati wa mchakato wa ukaguzi, CAG tayari anakusanya majibu kwa kila hoja ya ukaguzi, na hivyo kazi ya serikali ya kuandaa majibu inakuwa suala la majumuisho tu.


Kwa kutekeleza hatua hizi, CAG ataweza kuwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa rais ifikapo tarehe 31 Januari, na kuruhusu kuwasilishwa katika kikao cha Bunge la Februari pamoja na majibu ya serikali. Kwa hiyo, kikao cha Bunge cha Februari kinaweza kutoa maagizo kwa serikali; na serikali itatakiwa kutoa taarifa ya utekelezaji katika kikao cha Bunge cha 'Aprili - Juni', yote ndani ya mwaka huo huo wa fedha. Taarifa ya serikali ya utekelezaji wa maagizo ya bunge kuhusu Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pia itakuwa ni mchango muhimu katika michakato ya uidhinishaji wa bajeti itakayofanyika katika kikao hicho.


Kielelezo hapa chini kinaonyesha muda utakaochukuliwa kwa ripoti ya ukaguzi kujadiliwa na bunge utapunguzwa kutoka miezi 17 hadi miezi 8. Zaidi ya hayo, ndani ya miezi 10, taarifa ya utekelezaji ya serikali itakuwa imewasilishwa bungeni kama mchango kwenye mchakato wa kuandaa bajeti.

In the proposed timeline, the time taken for the audit findings to be discussed by parliament would be reduced from 15 months to 8 months. Additionally, within 10 months, the government's implementation report would be presented to parliament as an input to the budget preparation process.

Ingawa uwezekano utategemea na mambo mengine na kuna umuhimu wa mabadiliko ya sheria na kanuni, utekelezaji wa hatua hizi utaboresha kwa kiasi kikubwa umuhimu na manufaa ya ripoti za ukaguzi za CAG nchini Tanzania. Hii itapelekea kuongeza uwajibikaji, uwazi, na imani ya umma katika shughuli za serikali.

 

Kanusho:

Taarifa zilizotolewa katika makala haya na tafsiri yake kwa Kiswahili zimetokana na ripoti ya CAG ya mwaka 2022/23 na inaakisi tafsiri ya mwandishi na pia uchambuzi wake wa taarifa na takwimu. Ingawa jitihada zimefanywa ili kuhakikisha usahihi wa taarifa, mwandishi na mchapishaji hatawajibika kwa makosa yoyote, kuachwa au kutokuwa na usahihi. Wasomaji wanashauriwa kurejea ripoti halisi na vyanzo vingine rasmi ili kupata maelezo ya kina na sahihi. Maoni yaliyotolewa katika makala haya ni ya mwandishi na si lazima yaakisi sera rasmi au msimamo wa AGIM Consultants.

0 comments

Comments


bottom of page